Jeshi
la Polisi limekwepa kuwajibika kueleza kuhusiana na mchakato wa uchunguzi wa
tukio la kutekwa, kupigwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda. Aprili mwaka huu Jeshi hilo
liliahidi kwamba lingetoa taarifa kwa umma kuhusiana na uchunguzi wa timu
iliyoundwa kuchunguza tukio hilo. Hata hivyo, maofisa waandamizi
wameshindwa kutekeleza ahadi hiyo na kuunyima umma haki ya kujua waliotenda
uhalifu huo wa kinyama na hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Mara kadhaa,
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa
ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, wamekuwa wakikwepa kulizungumzia suala hilo na
kuahidi kuwa taarifa zitatolewa baadaye.
Kibanda
ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited ambayo
ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African,
alivamiwa na watu hao, wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es
Salaam Machi 5, mwaka huu. Jana NIPASHE iliwasiliana na Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai Nchini, Kamishna Robert Manumba, ambaye alisema hawezi
kulizungumzia kwa kuwa hakuwapo wakati kikosi kazi kilipoundwa na kuelekeza
aulizwe aliyekiunda. “Tume hiyo iliundwa lini?” alihoji na kuendelea:
“Aulizwe aliyeunda atakuwa na majibu sahihi, mimi siwezi kueleza
lolote.” Wakati kikosi hicho kinaundwa, DCI Manumba alikuwa nchini Afrika
Kusini kwa ajili ya matibabu na Mngulu ndiye aliyekuwa anakainu nafasi yake.
No comments:
Post a Comment