WABUNGE CCM WAWAKATAA
UPEPO mbaya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unazidi kuvuma,
safari hii wabunge wake wakimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri
watatu. Mawaziri wanaotakiwa kung’olewa ni Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na
Mafunzo ya Ufundi), Dk. Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na
Dk. Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Kama Rais
Kikwete atakubali kuwaondoa madarakani mawaziri hao, hii itakuwa mara ya pili
kwake kufanya hivyo. Mara ya kwanza ilikuwa Mei mwaka jana. Mwaka jana
Rais Kikwete aliamua kuwaengua madarakani baadhi ya mawaziri waliokuwa
wakiandamwa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uwajibikaji mbovu.
Miongoni mwa walioenguliwa mwaka jana ni Dk. Haji Mponda
aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mustafa Mkulo (Waziri wa Fedha),
William Ngeleja (Nishati na Madini na Ezekiel Maige (Maliasili na
Utalii). Msimamo huo wa wabunge wameutoa jana katika kikao baina yao na Rais
Kikwete kilichokuwa kikitathimini mwenendo wa chama na utendaji wa
wabunge. Chanzo chetu ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa baada ya Rais
Kikwete kutoa hotuba ya ufunguzi, baadhi ya wabunge walianza kuchangia, huku
wengine wakishutumiana kwa kuvujisha siri za vikao nje kwa waandishi wa
habari. Wabunge hao walidai kuwa mawaziri hao watatu wamekuwa mzigo kwa
Serikali ya CCM kutokana na utendaji wao kutokuwa wa kuridhisha.
Walisema matunda ya uwepo wa mawaziri hao kwenye wizara husika
hayaonekeni, hivyo kumtaka Rais Kikwete awang’oe. Waziri Kawambwa
analaumiwa kwa kuzembea kwenye sekta ya elimu ambayo inazidi kushuka kiasi cha
kuifanya serikali ifute matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana. Walisema
kufutwa kwa matokeo hayo ambayo asilimia 60 ya waliofanya mtihani walipata
daraja sifuri, kunadhihirisha uwezo mdogo wa Dk. Kawambwa. Wakati Kawambwa
akibanwa kwa hilo, wenzake Mathayo na Mukangara wanadaiwa kuwepo wizarani bila
kuonesha ufanisi wowote.Wabunge hao walidai kuwa Wizara ya Mifugo na Maendeleo
ya Uvuvi anayoiongoza Dk. Mathayo ni nyeti na ilipaswa kuwa ya pili katika
kuchangia pato la taifa baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walimshambulia Dk. Mathayo kuwa mzigo kwa wizara hiyo kwani
alipokuwepo Dk. Magufuli (Waziri wa Ujenzi) ilikuwa ikifanya vizuri tofauti na
hivi sasa. “Tusioneane aibu, huyu Mathayo ameshindwa kazi, mwenyekiti
muondoe kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya,” alisema mbunge mmoja.
JK abariki mchakato wa urais
Mapema katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Rais
Kikwete aliruhusu makundi ya wana-CCM wanaotaka kuwania urais 2015 kuendelea na
mchakato wa kuweka mikakati yao ya kampeni bila chuki. Kwa mujibu wa
chanzo chetu katika kikao hicho ambacho waandishi hawakuruhusiwa kuingia, lengo
kubwa lilikuwa ni kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwemo utekelezaji wa
ilani ya uchaguzi katika majimbo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ahadi za
rais. Rais Kikwete aliwataka wana-CCM wenye nia ya kugombea urais
kuendelea na mikakati yao kwa ustaarabu na kuepusha uadui kutokana na wapambe
wao kuwa na kambi zaidi ya moja.
“Tuangalie makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja
chama, wenye nia hiyo ya kugombea waendelee na mikakati yao na si kujenga chuki
kwa makundi mengine. “Mkumbuke kuwa kambi hizo za urais zinatakiwa kujitizama
na wafuasi wao maana wafuasi wengi si wa kuaminika,” alisema Kikwete. Rais
Kikwete aliwafananisha baadhi ya wapambe na matango pori yanayoota popote,
ambapo alisema wamekuwa na tabia ya kutoa maneno huku na kupeleka upande wa
pili. Tanzania Daima ilidokezwa kuwa Kikwete alikuwa na ajenda nne ambazo
ni urais 2015, kuwahimiza wabunge kutembelea majimbo yao ya uchaguzi, kurudi
majimboni kwao kusimamia ahadi zao, chama na zile za viongozi wa kitaifa
akiwemo yeye na kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa.
Kwamba Kikwete aliwataka wabunge hao kutumia kauli za staha
wanapoikosoa serikali kama ambavyo baadhi wamekuwa wakifanya. “Mnatakiwa
kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna baadhi yenu mmekuwa
mnaibomoa serikali kwa jinsi mnavyochangia huko bungeni, hilo si jambo jema
hata kidogo, waachieni wale wenzenu,” alisema. Katika hilo, wabunge
walionya tabia ya baadhi ya mawaziri wanavyohusiana na wabunge na
wanavyoonekana kwa wananchi, lakini wakaitaka serikali kutimiza wajibu wake
ipasavyo kwa kutoa fedha za bajeti kama zinavyopitishwa na Bunge.
Pia ubadhirifu unaofanywa kwenye halmashauri nchini, utendaji
mbovu wa baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa nchini, hivyo wakamtaka rais
kukunjua makucha yake kuondokana na uozo huo.
Kuhusu kutembelea majimbo, rais alisema kuwa baadhi ya wabunge
wameyatelekeza kwa kutorudi kusikiliza kero za wananchi na kutimiza ahadi
zao. Aliwaonya kuwa kwa tabia hiyo wala wasije kuwaonea donge wale
wanachama wengine watakaochaguliwa kuwa wabunge badala yao.
Lugola, Filikunjombe, Mpina wakaangwa
Baada ya mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa
wabunge kutoa madukuduku yao ambapo chanzo chetu kinasema kuwa wabunge watatu
walishambuliwa kwa tabia yao ya kuikosoa serikali kwa kauli nzito. Wabunge
hao ni Kangi Lugola (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa) na Luhaga Mpina wa
Kisesa ambao hata hivyo wote hawakuhudhuria kikao hicho. Lugola amekuwa
mwiba mkali wa kuwashambulia mawaziri wa serikali kutokana na utendaji wao
kutoridhisha ambapo hivi karibuni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), alitishia kuwataja mawaziri na watendaji
wanojihusisha na rushwa pamoja na biashara ya dawa za kulevya.
Filikunjombe naye amekuwa akipinga kuunga mkono hoja za serikali
huku akitumia maneno makali kama vile ‘serikali kuvaa miwani ya mbao’, kutokuwa
sikivu na mengine kama hayo ambayo inaelezwa kuwa hata Rais Kikwete jana
aliyatolea mfano.
Chanzo chetu kilieleza kuwa aliyeibua sakata hilo ni mbunge
mmoja wa Tabora, akidai wenzao hao wamekuwa na tabia isiyokoma, na hivyo
kupendekeza kuwa kama wanataka ni heri wakahamia upinzani kuliko kuendelea
kuivua nguo Serikali ya CCM. Hadi tunakwenda mitamboni jana, kikao hicho
kilikuwa kikiendelea na kwa mujibu wa ofisa mmoja wa chama, walitarajia kuwa
kingemalizika usiku wa manane.
Source: Tanzani Daima (May 2013). Mawaziri watatu
kung’olewa. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment