MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) ametuma salaam za pole na rambirambi kwa waumini wa
Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na mlipuko
uliotokea katika Kanisa la Olasiti, Jijini Arusha, uliosababisha vifo na
majeruhi, huku wengine wakipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo.
Mwenyekiti Mbowe ametoa salaam hizo
alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC),
Padri Antony Makundi, jioni ya Jumapili, baada ya kupata taarifa za tukio la
mlipuko huo unaodhaniwa kuwa ni bomu.
"Tumepokea habari za tukio la
mlipuko uliotokea leo (jana) katika Kanisa la Olasiti huko Arusha kwa mshtuko
na masikitiko makubwa. Kupitia kwako tunapenda kutoa pole kwa familia, ndugu,
jamaa na waumini wa Kanisa la Olasiti waliopatwa na msiba, waliojeruhiwa na
wengine waliopatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo lisilokuwa la
kawaida.
"Tunapenda pia kupitia salaam
hizi, kuwapatia pole waumini wote wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote
walioguswa na tukio hili la leo (jana). Mwenyezi Mungu awajaze imani, nguvu na
kuwapatia moyo wa subira nyote, wakati huu mgumu wa majonzi mazito na
kutafakari tukio hilo.
"Tumuombe awajalie uponyaji wa
haraka na ahueni na afya njema wale wote waliojeruhiwa na waliopatwa na mshtuko
kutokana na tukio hilo. Kupitia kwako pia naomba utufikishie salaam zetu za
pole kwa Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalemkutwa kwa niaba ya uongozi wa
Kanisa Katoliki nchini," alisema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe, ambaye pia ni
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) aliwataka Watanzania wote kuwa
watulivu wakati huu, wakati ambapo serikali kupitia vyombo vya dola inafanya
uchunguzi wa tukio hilo. Alisema serikali haina budi kuchunguza na kutoa
taarifa za matukio mengine yote ya namna hiyo ili kuwahakikishia Watanzania
wote haki na matumaini ya kuendelea kuishi kwa utulivu katika nchi yao.
Imetolewa leo Mei 6, 2013,Dar es
Salaam na;
Kurugenzi ya Habari na Uenezi
Makao Makuu ya CHADEMA.

No comments:
Post a Comment