Nimefuatilia leo asubuhi juu ya
maneno niliyotamka Olasiti Kanisani baada ya bomu , nimeona michango mbali
mbali katika mitandao ya jamii , nawapongeza wale wenye kutambua ukweli na
kuutetea ukweli lakini pia wale wasiojua ukweli lakini wamefanikiwa kupata
maarifa ya kujua matumizi ya kompyuta kwa hiyo nakusikia fahari kuandika maoni
yeyote wanayotaka , Watu hawa ni muhimu kwani wanasaidia kutambua kwa wepesi
kuwa sio kila mtu anayeweza kutumia Internet ni mwenye uelewa na akili , hivyo
inasaidia Wazazi kujua namna ya kusaidia watoto wao katika siku zijazo. Maneno niliyotamka ni muhimu sana ,
NUKUU , “ Nawapa pole wote mliofikwa na majanga haya , Mimi nichukue fursa hii
kuwapa pole , lakini niwe jasiri sana kusema ukweli kama ninyi waandishi wa
habari hamtafanya editing…..
“ Kwanza kabisa niweke wazi kuwa
jambo hili limesababishwa na chokochoko za udini ambazo muasisi wake ni
Serikali ya CCM na viongozi wake, aliyepiga bomu hapa leo siyo jambazi wa
kutaka mali bali ni mtu aliyeelewa na kufundishwa tofauti kwa nia mbaya kuhusu
dini nyingine, haya maneno ya udini yalianzishwa na viongozi wa Chama tawala
lengo likiwa ni kuwagawa na kuwatawala raia lakini kwa sasa wamelikoroga,
wamewachonganisha watu wa dini mbalimbali hasa Waislam na wakristo ambao ndio
wengi katika taifa hili bila kujua madhara ya mkakati huu kuwa utaligawa Taifa. Sasa basi kazi hiyo waliyoifanya
haya ndio mavuno yake kwani tukio hili lina sura zote za kiimani na kigaidi na
nilitake jeshi la polisi kufanya kazi ya kuwakamata haraka kama ambavyo
walinikamata mimi nyumbani kwangu kwa mabomu na vitisho , nawapa pole sana watu
wote mliopatwa na janga hili .
Niliposema maneno haya ni maneno ya
msingi kwa wakati muhimu , watu wameumizwa na wengine wamekufa na sababu ni
uchochezi ulionza muda mrefu kufanywa na Chama tawala Wakati siasa ya udini na
ukabila na Ukanda zinafanywa iliwafurahisha watawala kwani lengo lao la Wagawe
na watawale lilifanikiwa bila kujua matokeo yake ni mabaya kiasi gani . Tukio
la Jana Olasiti Arusha sio la kijambazi ni mgongano wa imani ambao watawala
wanataka kuuzima kwa propaganda badala ya kujadili ukweli wa hali halisi ili
kutibu jeraha hili baya ambalo halita muacha Mtu yeyote salama .
Kuna mambo mengi yanaendelea katika
jambo hili linalohusu udini katika Taifa letu na ushauri wangu kwa Serikali ni
kwamba hawawezi kutibu Malaria kwa kumeza panadol kuogopa kusema ukweli sio
uzalendo bali ni ujinga , tena ujinga mkubwa sana , Malcom X alisema “ Huwezi
kuwa mzalendo kiwango cha kupuuza ukweli na kujifanya hauoni , Leo hii ndivyo
watu wanavyotaka kufanya katika jambo gumu kama hili , swali muhimu sana ,ni
nani kati ya Mkristo au Mwislamu atakayekwenda kusali kwa amani kama vitendo
hivi visipo kemewa kwa ukweli na kuweka bayana mzizi wa jambo hili la uvunjifu
wa amani ambalo tiyari kuna Sheikh alimwagiwa tindikali kule Zanzibar na
matukio mengi kama haya ambayo yamewapata Mapadri na Wachungaji , hivi kweli
katika Taifa hili tunafika mahali tutaanza kuingia katika Nyumba za Ibada kwa
kufanyiwa upekuzi kama tunasafiri kwenda Marekani? kwani inavyoonekana huko
ndiko tunakoelekea, ieleweke kwamba jambo hili litakwenda kupunguza idadi ya
watu kwenda kuabudu na mwisho wahalifu wataongezeka kwani kazi ya Msikiti na
Kanisa ni kufundisha watu nia njema dhidi ya uovu ambao ni chukizo kwa Mungu
ambapo mafunzo haya hayapatikani kwingine kokote kirahisi isipokuwa huko ni
vyema watu wakajifunza kusema ukweli kwani hakuna namna unaweza kupata uhuru
kamili bila kuwa mkweli .
Wachungaji na Maaskofu wanajua pale
Chama Tawala kiliposema CUF ni chama cha Udini tena Waislamu na Watu wote
wanaona na kusikia pale Chama Tawala kinaposema kuwa Chadema ni Chama cha
Wakristo , limeonekana ni jambo la kawaida sana bila kutafakari madhara yake na
sasa haya ni madhara makubwa ya siasa yenye lengo la “ Wagawe halafu watawale “Ni Jambo la kusikitisha kama
mgogoro huu wa Udini utashindwa kujadiliwa kwa makini na badala yake kutafuta
propaganda za kuzima jambo hili , mtaweza kufanikiwa kwani nyie ni Serikali na
mnazo njia nyingi za propaganda lakini ukiona unafanikiwa kufanya jambo baya
bila kuyumba basi tambua mwisho wake ni mbaya na mkubwa sana , Hekima sio
kukwepa ukweli , hekima ni kujadili ukweli , hekima sio kuita viongozi wadini
Ikulu, hekima ni kuacha Siasa chafu kwa vitendo na kutubu dhambi kubwa ya
kuwagawa Watanzania ambayo mmekwishaifanya .
Niliposema CCM na Rais Kikwete ndio
kinara wa Udini mlinibeza bila hata kuona ushaidi wangu na hata mimi
nilishangaa sana huo ujasiri wa kunibeza mliupata wapi bila hata kujua ni kitu
gani ninacho kama ushahidi , sio kazi nyepesi kumtuhumu Rais kwa kiwango hicho
na wala sio jambo jepesi pia kusema maneno hayo , kwani Rais ndio mwenye
mamlaka ya vyombo vyote vya usalama katika Taifa letu , ni hatari kubwa ambayo
inaweza kufupisha maisha yangu lakini tunajipa moyo tukijua kuwa hakuna Mtu
hatakayeishi milele , familia zetu zinaishi kwa mashaka lakini tunavumilia
matusi , mateso , udhalilishwaji , kebehi na vitisho kwa ajili ya siku zijazo
za Nchi yetu na watoto wetu .
Kuna tatizo kubwa Tanzania
linahitaji hekima na ujasiri na propaganda za CCM hazitaweza kutibu tatizo hili
isipokuwa unyenyekevu wa hali ya juu na kukubali kuwa lipo tatizo na chuki
zinaendelea kusambaa siku hadi siku na kama mtapuuza iko siku mtasema
tuliambiwa na haya maandishi yangu sio ya mara ya kwanza kuandika kuhusu Udini
, naogopa sana kuishi kwenye nchi ambayo watu wataheshimiana kwa dini na kabila
zao na sio utu wao na ubinadamu .
Miaka ya nyuma tuliishi vizuri sana
tu na Chama tawala mlipoona mnatoka madarakani mlitumia propaganda za Udini na
Ukabila , lakini pia baadhi ya viongozi wa Dini wamekuwa wakitumika vibaya pale
wanapofikiri na kujua kuwa Wanasiasa wanaweza kuchangia vyema katika mambo
mbali mbali ya maendeleo ya taasisi za Kidini hapo ndipo mnapotoa mwanya wa
Wanasiasa kufanya siasa za udini , hivi kweli nini kinawapa ujasiri baadhi ya
Viongozi wa dini kuamini kuwa Wanasiasa wanaoishi kwa mshahara wanaweza kuwa
matajiri wakubwa wanaochangia mamilioni ya fedha. Hili nalo ni tatizo ,
Viongozi wa kisiasa kuzunguka kwenye nyumba za Ibada kila kukicha ili kutafuta
thamani ya kuungwa mkono katika matarajio yao , ili Viongozi wadini wawe na
mamlaka ya kuisadia Serikali wajue kwamba wanahitaji kutambua mamlaka
waliyonayo katika shughuli zao lakini Mbunge au Waziri au Kiongozi yeyote wa
Kisiasa anapokuwa na heshima kuliko Viongozi wa Dini ni dhahiri kuwa Mamalaka
yao imepotea nalo hili ni tatizo kubwa sana kwani kazi kubwa ya Viongozi wa
dini ni kusimamia haki , kukemea maovu na kukosoa na vile vile kusaidia
Viongozi wa Serikali kutenda kweli na sio kugeuza Nyumba za ibada kuwa maficho
ya Viongozi waovu .
Mwanafalsafa maarufu wa Kiyahudi
Elie Wiesel alisema, “there may be times when we are powerless to prevent
injustice, but there must never be a time when we fail to protest.” Kwa
Kiswahili, “kuna nyakati tunaweza kuwa wadhaifu katika kuzuia uovu na dhuluma,
lakini kamwe isijetokea wakati ambapo tutashindwa kupinga uovu na dhuluma.” Lakini pia , Frederick Douglass
zaidi ya miaka mia moja na hamsini iliyopita alisema “he is a lover of his
country who rebukes rather justify its sins”, yaani, “mpenzi wa nchi ni yule
anayekemea madhambi yake badala ya kuyahalalisha”! Nawapongeza pia Wananchi wote
waliokubali kujitolea Damu baada ya Mimi na Mbunge mwenzangu kuhamasisha jambo
hilo ambalo limebeba utu mwingi , asanteni sana na Mungu awabariki sana na wale
ambao hamkutoa Damu kwa sababu vifaa viliisha tafadhali naomba sana siku ya
Jumatano mkajitolee damu katika uwanja wa Abeid Karume .
“ Dhambi kubwa na mbaya kuliko zote
Duniani ni Uoga “
GODBLESS J LEMA (MP)

No comments:
Post a Comment